Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, moja ya nyenzo muhimu ya kuleta usawa katika maisha ya mwanadamu ni kuzingatia kifo.
Amirul-Mu’minin (a.s.) anasema:
«أَلَا فَاذْکُرُوا هَاذِمَ اللَّذَّاتِ وَ مُنَغِّصَ الشَّهَوَاتِ وَ قَاطِعَ الْأُمْنِیَاتِ.»
Tambueni! Kumbukeni kifo ambacho ni mharibifu wa ladha, mvunja matamanio na mkataji wa matumaini. (1)
Sherehe:
Maisha ya mwanadamu yamejaa matamanio na ladha.
Mwanadamu hakukatazwa kuwa na matamanio au kufurahia ladha za dunia, bali onyo ni kwamba yasije yakamtoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ili kuzuia hilo, mwanadamu anahitaji chombo kitakachomuweka katika usawa kati ya raha na matatizo ya maisha, na asitengane na Mwenyezi Mungu.
Moja ya nyenzo bora zaidi zilivyotajwa kwa lengo hili ni yakin na imani ya kweli juu ya kifo.
Ikiwa utakuwa tajiri, kukumbuka kifo kutakuepusha na majivuno na kukufanya uone kila kitu ni cha Mwenyezi Mungu, hivyo mali yako itaelekezwa kwenye matumizi ya kheri.
Ikiwa wewe ni maskini, kukumbuka kifo kutaizuia roho yako kuhisi wivu kwa mali ya matajiri.
Kama Mtume Muhammad (s.a.w.w.) anavyosema:
«فإن ذَکَرتُموهُ عِندَ الغِنی هَدَمَهُ، و إن ذَکَرتُموهُ عِندَ الفَقرِ أرضاکُم بعَیشِکُم.»Mkimkumbuka kifo wakati wa utajiri, kinaharibu (majivuno yenu), na mkikumbuka wakati wa umasikini, kinakuridhisheni na maisha yenu. (2)
Ikiwa mtu ana yakini kwamba siku moja kifo kitampambanua kati yake na jamaa zake, hatakuwa tayari kumkasirisha Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwapendeza wao.
Na iwapo anaamini kwamba kifo kitamuwekea ukuta kati yake na ladha za kidunia, atazidhibiti ladha hizo ndani ya mipaka ya ridhaa ya Mwenyezi Mungu.
Na akiamini kwamba kifo kitakata ndoto zake, basi ndoto yake kuu itakuwa ni radhi za Mwenyezi Mungu.
Kwa hakika, matatizo mengi ya kiroho ya mwanadamu yanatokana na namna anavyoiona dunia na mambo ya kidunia. Chombo kinachoweza kusahihisha mtazamo huo ni kuzingatia kifo.
Kama Imam Ja‘far Sadiq (a.s.) anasema:
«ذِکْرُ الْمَوتِ ... یُحَقِّرُ الدُّنْیا.»Kukumbuka Mauti huifanya dunia kuwa duni na isiyo na thamani. (3)
Wakati dunia inapodhoofika machoni kwa mtu, macho yake hugeuka kuielekea Akhera – na mara nyingi pale ndipo mwanzo wa ibada ya kweli. Lakini pale dunia inapokuwa kubwa na yenye thamani machoni pake, haiwezekani kuanza safari ya utumwa kwa Mwenyezi Mungu.
Amirul-Mu’minin (a.s.) katika kuwa kusifia muttaqin (wachamungu) anasema:
«عَظُمَ الْخَالِقُ فِی أَنْفُسِهِمْ فَصَغُرَ مَا دُونَهُ فِی أَعْیُنِهِمْ.»Muumbaji amekuwa mkubwa ndani ya nafsi zao, na kwa hiyo kila kitu kisicho Yeye kimekuwa kidogo machoni mwao. (4)
Rejea:
1- Nahjul-Balagha, hotuba ya 99.
2- Tanbih al-Khawatir wa Nuzhat al-Nawazir, j. 1, uk. 269.
3- Bihar al-Anwar, j. 6, uk. 133.
4- Nahjul-Balagha, hotuba ya Muttaqin.
Imeandaliwa kutoka katika kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako